Genesis 22

Kujua Uthabiti Wa Ibrahimu

1 aBaadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!”

Ibrahimu akajibu, “Mimi hapa.”

2 bKisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaka umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

3 cIbrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. 5 dAkawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”

6 eIbrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7 fIsaka akanena akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!”

Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”

Isaka akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”

8 gIbrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.

9 hWalipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 iKisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11 jLakini malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

12 kAkamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”

13 lIbrahimu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 mIbrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire.
Yehova-Yire maana yake Bwana atatupa.
Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima wa Bwana itapatikana.”

15 oBasi malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 pakasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 qhakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 rna kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”

19 sNdipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer-Sheba. Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.

Wana Wa Nahori

20 tBaada ya muda, Ibrahimu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto, amemzalia ndugu yako Nahori wana: 21 uUsi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye, Kemueli (baba wa Aramu), 22 vKesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.” 23 wBethueli akamzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori nduguye Ibrahimu hao wana wanane. 24 xSuria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alikuwa na wana: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.
Copyright information for SwhKC